Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameeleza alichodai kuwa ni sehemu ya maswali na majibu kati yake na jeshi la polisi kuhusu sakata la kutekwa kwa Mohammed Dewji.
Kupitia akaunti yake ya Twitter, Lema ambaye leo alijisalimisha polisi kwa ajili ya mahojiano, amesema kuwa aliulizwa kuhusu kauli zake juu ya sakata hilo.
“Polisi wameniuliza maswali juu ya utekwaji wa Mo. Nimesema kuwa kutekwa kwa Mo na kupatikana kwake kumeacha wasiwasi mwingi. Naamini kama biblia ingekuwa bado inaandikwa pengine suala hili lingeandikwa kama muujiza,” ameandika.
Lema aliripoti katika makao makuu ya jeshi la polisi jijini Arusha majira ya saa nne asubuhi, akiitikia wito wa jeshi hilo ambapo alihojiwa.
Mbunge huyo ambaye ni waziri kivuli wa mambo ya ndani (Chadema), alizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita kuhusu sakata hilo ambapo anadaiwa kutoa kauli tata zilizosababisha jeshi hilo kuonya mihemko ya kisiasa dhidi ya kazi hiyo ya kipelelezi ambayo ni ya kitaalam.
Mwananchi wameripoti kuwa mbunge huyo aliulizwa katika mahojiano hayo na jeshi la polisi, ‘kwanini alitoa kauli ya kutaka wapelelezi kutoka nje ya nchi’.
Mo alipatikana Oktoba 11 mwaka huu kutokana na juhudi za jeshi la polisi lililomsaka kila kona hususan eneo la fukwe za bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kuonesha picha ya gari lililotajwa kutumiwa na watekaji hao.