Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wikendi iliyopita alitumia muda wake kufanya mazungumzo na kada mpya wa chama hicho, Wema Sepetu ikiwa ni siku mbili tangu aachiwe kwa dhamana baada ya kukaa gerezani kwa takribani miezi minne.
Lema alimtia moyo na kumpa somo mrimbwende huyo, akimtaka kuwa imara na kujitoa bila kujali ni watu wangapi wanaomuunga mkono.
“Hatuhitaji taasisi kupigania righteousness (haki), tunahitaji watu makini ndani ya taasisi. hauhitaji kampani kubwa sana, unahitaji commitment (dhamira), sacrifice (kujitoa) na determination (uamuzi wa ari).
Lema alimtaka Wema kufikiria vitu vikubwa zaidi na kuwa na ndoto kubwa hata ya kuwa rais wa nchi siku moja.
“Wewe unaweza kuwa kitu cha ajabu, unaweza hata kuota kuwa Rais wa nchi hii… nani ajuaye?” alisema.
Mbunge huyo machachari alimtaka Wema kujichukulia kama mwanamke shupavu na kusahau yaliyopita huku akimtia moyo kuwa hata kesi aliyofunguliwa mahakamani itakwisha pia.
Wema alitangaza kujiunga na Chadema akitokea CCM siku chache baada ya kutoka katika selo za polisi jijini Dar es Salaam alipokuwa akishikiliwa kwa siku zaba akituhumiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi. Alifunguliwa kesi baada polisi kudaiwa kukukuta msokoto wa bangi nyumbani kwake baada ya kumfanyia upekuzi.