Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuhusu hali ya uchumi anayoitarajia.
Akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam na wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini, Rais Magufuli alisema kuwa anatamani anapoondoka madarakani Tanzania iwe na mabilionea 100.
Lema ametumia mtandao wa Twitter kuelezea mtazamo wake kuhusu kauli hiyo. Mbunge huyo ameeleza kuwa kauli ya Rais inaleta matumaini na ina thamani kubwa.
“Kauli ya Rais kuwa anataka kuona Tz ya mabilionea100 kabla ya utawala wake ni kauli ya matumaini kwa Nchi. Kauli hii ina thamani kubwa kuliko ile ya matajiri kuishi kama mashetani. Nimemsikiliza Rais naona kama anasisitiza uwepo wa utawala bora/sheria ktk ngazi zote za Serikali.”
Rais Magufuli jana aliwaeleza wafanyabiashara nia nzuri ya Serikali ya kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora zaidi huku akiwasihi kuzingatia sheria na kulipa kodi kwa uaminifu.
Alipokea mawazo na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao. Baada ya kikao hicho, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph George Kakunda na kumteua Innocent Lugha Bashungwa kuchukua nafasi hiyo.
Aidha, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Edward Kichere na nafasi yake ikachukuliwa na Edwin Mhede.