Hatimaye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) leo amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka mawili, ikiwa ni siku tatu tangu akashikiliwe na jeshi la polisi na kugoma kula chakula akitaka afikishwe mahakamani.

Lema amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili tofauti ambayo yote yametajwa kuwa ya kichochezi.

Katika shtaka la kwanza kwanza, Lema anatuhumiwa kumtumia ujumbe wa uchochezi Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambao ulikuwa na maneno, “Karibu tutakudhibiti kama mashoga wanavyodhibitiwa Uarabuni.”

Kadhalika, mwanasiasa huyo amesomewa shtaka la pili la kuandaa na kuhamasisha kufanyika kwa maandamano ya Septemba 1 yaliyopewa jina la ‘UKUTA’ na Chadema, maandamano ambayo Wakili wa Serikali, Vincent Njau ameeleza kuwa ni kinyume cha sheria.

Mbunge huyo alikana mashtaka yote mawili na mvutano ukaibuka katika kudai dhamana yake baada ya upande wa Mashtaka kuitaka Mahakama kuizuia kwa sababu walizoeleza kuwa ni za kiintelijensia na usalama wake.

Hata hivyo, Hakimu alitupilia mbali ombi la upande wa Mashtaka na kuruhusu Mbunge huyo kupewa dhamana huku akiipangia tarehe nyingine kesi hiyo.

Majaliwa akaribisha wawekezaji kutoka nje
Rais Malinzi Atuma Salamu Za Rambirambi Msiba Wa Munishi