Madiwani wawili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Kata za Terati na Daraja mbili Jijini Arusha wamejiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Madiwani hao ni pamoja na Prosper Msofe (Daraja mbili) na Obeid Meng’oriki (Terati) ambao kwa pamoja wamesema kuwa wameamua kujiunga na CCM ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli.
Diwani mmoja kati ya waliohama amesema; “Hakuna maisha magumu ya kisiasa kama kuishi kwenye Ukoo wa kambale ambao Baba, Mama na watoto wote wana ndevu
Pia ameongeza kuwa; “Agenda hakuna, kila Mtu mropokaji na kulazimishana kufanya siasa za kuhujumu maendeleo kama njia ya kuijenga CHADEMA badala ya Nchi”
Aidha, Msofe ambaye aliwahi kuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha (CHADEMA) amesema kuwa sababu kubwa ya kuhama kwao ni Mbunge wa jimbo hilo Godbless Lema kuwapiga vita watu wenye uwezo mkubwa wa kuongoza ndani ya chama hicho.
Kwa upande wake, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Terati, Meng’oriki amesema kuwa CHADEMA ni chama cha kihalifu, kifitini na kilichojaa chuki, ubaguzi, na urasimu mkubwa huku akidai endapo ikitokea makada wa chama hicho wakimsifia Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya huwa wanakemewa vibaya.
Hata hivyo, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha Mjini, Musa Matoroka amesema kuwa madiwani hao wameamua kujiunga na Chama hicho ili kumuunga mkono Rais na kuahidi kushirikiana na wananchi.