Katika kuhakikisha kuwa anatoa ushirikiano wa kutosha kwa wanafunzi watatu walionusurika katika ajali ya iliyotokea Jijini Arusha, Mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless Lema ametoa shukrani zake kwa Mbunge, Lazaro Nyalandu kwa kufanikisha safari ya Marekani ya watoto hao watatu ambao walinusurika kifo katika ajali ya basi la shule ya Lucky Vicent iliyotokea Karatu na kusababisha vifo vya watu 35
Aidha, tangu itokee ajali hiyo, Nyalandu amekuwa bega kwa bega na kufuatilia kila hatua ili kuhakikisha watoto hao pamoja na wazazi wao na daktari wanasafiri kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
“Mh Lazaro Nyalando , Mungu akubariki sana kwa kazi nzuri ya kusaidia watoto waliopatwa na ajali hapa Arusha, jitihada zako Mungu atakulipa” amesema Lema.
Katika hatua nyingine, Nyalandu ameomba pesa zitakazo endelea kuchangwa na Watanzania na watu wengine duniani kwa ajili ya watoto hao zitumike kujenga ICU katika hospitali ya Mount Meru ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Arusha na mikoa jirani pindi linapotokea tatizo kama hilo.
“Kwa kuwa wadau wanaendelea kuchangia na kwa kuwa shule ya sekondari zimekubali kuanzisha mfuko ambao wanausimamia wenyewe na kwa kuwa mfuko huo lengo lao kubwa lilikuwa kuwasafirisha hawa watoto kazi ambayo imefanywa na Samaritan Purse, lakini lengo la pili ilikuwa ni kwenda kuwatibu kazi ambayo inafanywa na Shirika la STEMM kwa kushirikiana na Hospitali kuu ya Mercy hivyo kazi itakayobaki Mkuu wa Mkoa itakuwa ndogo, kwa hiyo nimeomba na nimeshaurina nao na wamekubali kwamba Watanzania na wanadunia wote watakao endelea kuchanga fedha zote ziletwe kwako Mkuu wa mkoa ili ziweze kujenga kituo cha wagonjwa ambao wanahitaji huduma ya haraka (ICU) katika hospitali yetu ya Mount Meru” amesema Nyalandu.