Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyofuatilia mwenendo wa Opereshini Tokomeza baada ya kuwepo kashfa kuwa ilisababisha mauaji na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi wasio na hatia, James Lembeli ameweka wazi jinsi alivyotaka kulaghaiwa kwa fedha.

Akiongea katika Mkutano wa Chadema kanda ya ziwa baada ya kutambulishwa rasmi kwa wananchi kuwa mwanachama mpya wa chama hicho, Lembeli alisema kuwa baada ya kufanya uchunguzi kuhusu kashfa hiyo alifuatwa na upande wa serikali ambao ulitaka kumpa kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 50 ili asilipue maovu ya operesheni hiyo.

Hata hivyo, alisema busara zake na ushauri wa aliyekuwa mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM ambaye pia amehamia Chadema, Ester Bulaya, mpango huo ulishindikana na kila kitu kikawekwa wazi bungeni.

“Ester Bulaya alinisaidia sana, ngoja leo niwaambie. Walipoona hali sio nzuri, upande wa serikali walileta mapesa. Ester akaniambia, ‘mzee Lembeli shilingi milioni 50 itakusaidia nini katika maisha yako..’, akasema ‘kama miaka yote katika maisha yako ulishindwa kukusanya shilingi milioni 50 iweje leo’. Akanambia achana nayo hii hela, lazima tuwaambie wananchi Tokomeza iliwadhalilisha vipi wananchi’.”

Operesheni Tokomeza iliyolenga kuwasaka majangili na wote wanaoshirikiana na majangili hao katika kuua wanyama pori kinyume cha sheria, iligeuka kuwa kashfa nzito iliyowaondoa baadhi ya mawaziri katika nafasi zao baada ya kubainika kuwa maafisa waliowatuma katika operesheni hiyo waliwadhalilisha na kuwapa hasara kubwa wananchi wasio na hatia.

Kinda La Ghana Kucheza Soka Hispania
Hamad Rashid Aiunganisha CUF na CCM