Wakati dakika na sekunde zinazidi kusogea kabla dunia haijashuhudia mtanange wa kuchimba na sururu kati ya Juventus na Manchester United kwenye Ligi ya Mabingwa-Ulaya, timu hizo mbili zimetangaza taarifa za wababe wake uwanjani.
Meneja wa Manchester United ametangaza habari itakayowanyong’onyeza mashabiki wa timu hiyo, kuwa mshambuliaji Alexis Sanchez hataingia uwanjani leo dhidi ya Juve.
Mshambuliaji huyo ambaye aliingia katika dakika za majeruhi kwenye mchezo dhidi ya Chelsea Jumamosi iliyopita, ulioshuhudia timu hizo zikitoka sare ya 2-2, ameripotiwa kuwa majeruhi, kwa mujibu wa kocha Jose Mourinho.
Aidha, wekundu hao wa Old Trafford watamchezesha mlinzi wa ngome yao, Antonio Valencia kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2 alipolazimika kufanyiwa upasuaji wa mdomo kutokana na majeraha aliyoyapata.
“Alikuwa na matatizo na alifanyiwa upasuaji wa mdomo. Ndio sababu alihitaji muda wa kupata matibabu. Na hii ndiyo sababu hakuonekana kwenye mazoezi kwa siku kumi,” alisema Mourinho.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa Italia, Juventus wao wamepanga kuanza na kombora walilolisajili kutoka Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye alitumikia klabu ya Manchester kwa miaka 6, tangu 2003-2009.
Hii itakuwa mechi ya kwanza kwa Ronaldo tangu alipotolewa katika mchezo kati ya wababe hao na Valencia, Septemba 19.
Aidha, Ronaldo ambaye anakabiriwa na tuhuma za ubakaji, ametumia muda wake nchini Uingereza kuelezea sakata hilo akisema kuwa mwanasheria wake analishughulikia. Ameeleza kuwa tuhuma hizo ni za uongo na haziwezi kuathiri kwa namna yoyote kazi yake uwanjani.
Kama ilivyo kwa Man Utd kumkosa Sanchez, Juventus nao watalazimika kuwakosa mshambuliaji kutoka nchini Croatia, Mario Mandzukic, kiungo wa timu ya taifa ya Ujerumani, Emre Can pamoja na Sami Khedira.
Juventus wataingia uwanjani leo wakiwa kifua mbele kwani wanaongoza Kundi H kwa alama mbili mbele, baada ya kushinda michezo ya ufunguzi dhidi ya Valencia (2-0) na klabu ya Uswizi ya Young Boys (3-0).
Man Utd wao wataingia uwanjani kwa mtanange huu wa kihistoria tangu mwaka 2003, wakiwa nyuma kwa alama mbili.
Mourinho amekiri kuwa Juve wako vizuri zaidi yao kutokana na kuwa na mfumo mzuri, wachezaji wazuri pamoja na kocha aliyekaa kusuka timu hiyo kwa kipindi kirefu zaidi.
“Wameshashinda mataji saba na wana wachezaji wazuri ambao wanaweza kufanya mambo ya utofauti sana. Wao ni zaidi yashindani kwenye Ligi ya Mabingwa ,” alisema Mourinho.
Juve watawakabili Man Utd wakiwa hawajapoteza michezo 11 ya Ligi na Kombe katika msimu huu, wakiwa na sare ya 1-1 waliyoipata dhidi ya Genoa Jumamosi iliyopita.