Klabu ya Liverpool imeripotiwa kuwa, imeweka kipaumbele kumnasa winga wa Bayern Munich, Leroy Sane, awe mirithi wa Mohamed Salah ambaye anatarajiwa kutimkia Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa tovuti ya michezo ya The Mirror, Liverpool inajipanga kuvunja rekodi ya uhamisho katika historia ya klabu hiyo, kumnasa Sane.
Rekodi ya uhamisho katika klabu hiyo hivi sasa inashikiliwa na Darwin Nunez, aliyetua kwa Pauni Milioni 64.2 na nyongeza ya Pauni Milioni 21.4, akitokea klabu ya Benfica mwaka 2022.
Ikiwa mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, miamba hiyo italipa zaidi ya fedha ilizomnasa Nunez, ili kumsajili Sane.
Hata hivvyo, Bayern inaweza kuweka ngumu kumpoteza Sane ambaye amefunga mabao sita katika mechi saba za Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu 2023/24.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameripotiwa kuwa, anavutiwa na Sane na anataka kumrudisha katika michuano ya Ligi Kuu ya England (EPL).
Wakati alipokuwa akikipiga katika timu ya Manchester City, Sane alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya England, Kombe na FA na mataji matatu ya Kombe la Ligi.
Salah ameanza msimu huu kwa kiwango kizuri akifunga mabao matano na kutoa pasi nne za mabao katika mechi nane za Ligi Kuu ya England.
Inatarajiwa kuwa nyota huyo kutoka nchini Misri mwenye umri wa miaka 31, anaweza kutimka katika kikosi hicho Januari mwakani na kutimkia katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Nyota huyo alikuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa kwenda Saudi Arabia katika majira ya kiangazi mwaka huu, kufuatia klabu ya Al Ittihad kutuma ofa ya Pauni Milioni 150, lakini Liverpool ilipiga chini.
Nyota huyo aliyebakisha chini ya miaka miwili katika mkataba wake na Liverpool, anaweza kutimka katika kikosi hicho na kutua katika Ligi Kuu Saudi Arabia.
Katika kikosi cha Liverpool, Salah amecheza michezo 315 na kufunga mabao 192.