Shirikisho la soka nchini Libya (LFF) limekubali mualiko wa kushiriki fainali za mataifa bingwa barani Afrika (CHAN) zitakazounguruma nchini Cameroon mwezi Aprili.
CAF walituma mualiko LFF, baada ya kupata uhakika wa kujitoa kwa Tunisia kwenye fainali hizo, ambazo hushirikisha wachezaji wanaocheza kwenye ligi za ndani (ligi za mataifa ya barani Afrika).
Shirikisho la soka nchini Tunisia lililazimika kuandika barua ya kuiondoa timu yake ya taifa, kufuatia mgomo wa klabu zinazoshiriki ligi ya nchini humo, wa kutokua tayari kuwaruhusu wachezaji kwenda Cameroon kushiriki fainali za CHAN, ili hali ligi yao ikiwa inaendelea.
Sababu kubwa iliyotumiwa kwenye mgomo wa klabu za Tunisia, ni michuano ya CHAN kutokua sehemu ya kalenda la shirikisho la soka duniani FIFA, hivyo ni maamuzi yao kuwaachia wachezaji ama kuwakatalia, kujiunga na timu ya taifa.
Hata hivyo shirikisho la soka nchini Tunisia litalazimika kutoa dola 50,000 kama faini, kufuatia kuchelewa kuthibitisha kujiondoa kwenye fainali hizo, na taifa hilo limefungiwa kushiriki michuano ya CHAN kwa mwaka 2022.
Libya ambao walikua mabingwa wa CHAN mwaka 2014, walishindwa kufuzu kwenye fainali za mwaka huu, baada ya kufungwa na majirani zao Tunisia Libya jumla ya mabao matatu kwa moja.
Baada ya kuthibitisha ushiriki wa timu yao ya taifa, uongozi wa shirikisho la soka nchini Libya (LFF), umetoa ahadi ya kuiandaa vyema timu yao ili kuona inashiriki kwa kuonyesha ushindani mkubwa, na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa CHAN 2020.
“Tutakwenda kuonyesha kiwango cha hali ya juu, tunaamini maandalizi ya timu yetu yatakua mazuri na tutahakikisha tunafanya kila linalowezekana kutwaa ubingwa wa fainali za CHAN mwaka huu,” alisema katibu mkuu wa LFF Abdunnaser Ahmed.
“Kikosi chetu kitaweka kambi nje ya Libya kabla ya kuanza kwa fainali za CHAN, na tutajitahidi kuandaa mazingira mazuri kwa kila mchezaji ili kuwapa hali ya kujiamini.”
Tayari wenyeji wa fainali za CHAN 2020 (Cameroon) wameshataja miji itakayotumika kuni ni Yaounde, Limbe na Douala, huku viwanja vikiwa ni Japoma, Réunification, Ahmadou Ahidjo na Limbe.