Meneja wa klabu bingwa nchini England Manchester City Pep Guardiola, amempongeza Riyad Mahrez kwa kitendo cha ujasiri cha kuamua kupiga mkwaju wa penati, wakati wa mchezo wa jana jumapili dhidi ya Liverpool waliokua nyumbani Anfield.
Mahrez alichukua jukumu la kupiga mkwaju wa penati uliopatikana dakika tano kabla ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, baada ya beki wa Liverpool Virgil van Dijk kumuangusha Leroy Sane katika aeneo la hatari, na mwamuzi Martin Atkinson kufanya maamuzi hayo.
Guardiola aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kuwa, kila mmoja miongoni mwa wachezaji wake alikua na hofu ya kuchukua mpira na kwenda kupiga mkwaju huo, lakini Marrez alijikaza kisabuni na kujitwisha mzigo.
Amesema suala la kukosa kwake halina tatizo, kwani alitambua kuna matokeo ya aina mbili, kupata ama kusoka.
“Niliamini angeweza kupata, lakini ilikua bahati mbaya kwake, ninajivunia kuwa na mchezaji kama yeye, anajiamini na alionyesha ukomavu wa kutaka kuokoa jahazi la Man City ili lifanikishe ushindi katika mchezo wa leo (Jana), sina budi kumpongeza japo hakufanikiwa.”
“Mara kadhaa anapokua katika mazoezi, Mahrez hupiga penati nzuri na za kuvutia, ila katika soka kuna vitendo vya kustaajabisha sana, alipokosa nilihisi vibaya, lakini sikuwa na budi kukubaliana na hali halisi.”
Kiutaratibu mshambuliaji kutoka nchini Argentina Sergio Aguero huwa chaguo la kwanza kupiga mikwaju ya penati inayopatikana ndani ya dakika 90, lakini jana tayari alikua ameshatolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Gabriel Jesus.
Matokeo ya bila kufungana yameipa nafasi Man city kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi ya England kwa kuwa na faida ya uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, kwa upande wa alama (point) apo sawa na Liverpool na Chelsea, kwa kufikisha alama 20.