Michuano ya ligi daraja la kwanza kuanzia sasa itaanza kurekodiwa katika video kwaajili ya kumbukumbu zitakazosaidia kuondoa utata wa matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakilalamikiwa.
Hatua hiyo imetangazwa leo na bodi ya ligi inayohusika na uendeshaji wa ligi hiyo kufuatia malalamiko ya wadau wa soka kuhusu haki kutotendeka katika uchezeshaji wa michezo mbalimbali ya ligi hiyo.
Afisa Mtenda Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura, amesema kuwa haikuwa na utaratibu wa kurekodi mechi hizo, na pia wanahabari hawakuwa wakirushusiwa kuzirekodi kutokana na ligi yenyewe kutokuwa na televisheni maalum yenye haki ya kurusha ligi hiyo.
Amesema bodi hiyo itakuwa na kamati maalum kwaajili ya kurekodi mechi hizo kuanzia mechi zitakazopigwa mwishoni mwa wiki hii, lakini hazitaruhusiwa kurushwa kwenye kituo chochote cha televisheni.
“Haturekodi kwaajili ya kurusha kwenye TV, tunarekodi kwaajili ya kumbukumbu zetu,” amesema Wambura aliyekuwa akizungumza na wanahabari katika mkutano uliokuwa mbashara kupitia Azam Sports 2.
Bodi hiyo imefikia uamuzi huo ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa uamuzi wenye utata katika mchezo kati ya Dodoma FC na Alliance uliochezwa Desemba 30 mwaka jana katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma na kupelekea waamuzi hao watatu na msimamizi wa mchezo huo kufungiwa miaka mitatu huku Alliance ikipigwa faini.
Katika hatua nyingine, Wambura amesema licha ya waamuzi wa mchezo huo kuadhibiwa, matokeo ya uwanjani ambayo Alliance ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-2 yatabaki palepale kwa kuwa hakuna kanuni inayoelekeza kufutwa kwa matokeo kutokana na makosa ya waamuzi.
Miongoni mwa malalamiko ya wadau kuhusu mchezo huo, ni hatua ya mwamuzi kutoa kadi nne nyekundu kwa wachezaji wa Alliance, pamoja na waandishi wa habari kuzuiwa kuingia kwaajili ya kurekodi matukio muhimu ya mchezo huo, ambapo Wambura amewaomba radhi wanahabari wote waliokumbwa na kadhia hiyo.
Siku chache baada ya mchezo huo, waziri mwenye dhamana na michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliiandikia TFF barua akiitaka ichukue hatua dhidi ya malalamiko ya wadau wa soka kuhusu mchezo huo, na siku chache baadaye kamati ya saa 72 ilitangaza adhabu ikiwemo kuwafungia waamuzi wa mchezo huo.