Bodi ya Ligi (TPLB) imetangaza ratiba ya michezo ya viporo ya Ligi Kuu ya Tanzania na mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Juni 14 Uwanja wa Taifa, siku moja baada ya watani wao, Young Africans kumenyana na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amesema kwamba michezo ya viporo itaanza Juni 13 kwa Mwadui FC kuwakaribisha Young Africans Shinyanga na Coastal Union kuwa wenyeji wa Namungo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Juni 14, Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na Simba SC watawakaribisha Ruvu Shooting Dar es Salaam, wakati Juni 17, Young Africans watakuwa wageni wa JKT Tanzania Uwanja wa Taifa.
Kasongo amesema baada ya kukamilisha michezo hiyo ya viporo, rasmi Ligi Kuu itaanza Juni 20 na kufikia tamati Julai 26, mwaka huu.
Ligi Kuu ilisimama Machi 17, mwaka huu TFF kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.
Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza michezo 28, wakati vigogo, Young Africans ni wa tatu kwa pointi zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za michezo 28.
Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 michezo 28, Alliance FC pointi 29, michezo 29, Mbeya City pointi 30 michezo 29 na Ndanda FC pointi 31 michezo 29.