Muziki wa Afrika Mashariki umepata muamko mpya kufuatia uzinduzi wa tuzo kubwa za muziki zilizobatizwa jina la Mseto East Africa Awards (MEA) uliowashirikisha wawakilishi kutoka nchi tano za ukanda huo, ambapo Tanzania iliwakilishwa na mtangazaji wa Times FM, Omary ‘Lil Ommy’ Tambwe.
Tuzo hizo ambazo zimelenga kutambua pia sanaa nyingine mbali na muziki, zilizinduliwa kwa kishindo jana jijini Nairobi nchini Kenya ambapo kwa mujibu wa waandaaji ambao ni kampuni ya Mseto Company LTD, hazina uhusiano na chombo chochote cha habari na kwamba mchakato wa kuwachagua washiriki na washindi utafanywa kwa kuwashirikisha wawakilishi kutoka nchi zote tano ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.
Akizungumza ‘exclusively’ na Dar24, Lil Ommy ambaye yuko jijini Nairobi kwa ajili ya uzinduzi huo, amesema kuwa tuzo hizo zitaamsha ari mpya kwenye kiwanda cha muziki wa Afrika Mashariki kitakachowekwa pamoja. Pia, kutambua na kusherehekea mafanikio ya kazi za wasanii kuanzia mwaka huu.
Lil Ommy aligusia faida za kiuchumi pamoja na faida za sanaa ya muziki, kwani tuzo hizo zitafanyika kwa mzunguko katika nchi hizo, kila mwaka nchi moja ikipewa nafasi ya kuwa wenyeji (host).
“Zitakuwa na impact (matokeo) kubwa kwa sababu pia zitakuja kupita Tanzania, zitakuwa zinazunguka. Hivyo, pato la mji kama Dar litaongezeka kwa kuwa hotel, maduka ya nguo, malls vitakuwa bize. So, uchumi utapanda kwa wakati huo, sababu tuzo zitaleta wageni wengi kutoka pande mbalimbali. Lakini pia kuchangamsha muziki na kufanya wasanii wafanye kazi kwa bidii,” alifunguka.
“Muziki wetu utakuwa kwakuwa kuna platform (uwanja) ya kusherekea sisi wenyewe. Wasanii wanaofanya vizuri wataendelea na kazi kwa kuwa watakuwa wamepata ari na nguvu ya kupongezwa kwa kazi zao za sanaa,”aliongeza.
Pamoja na hayo, alisema kuwa kufanyika kwa tuzo hizo kubwa kutafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya wasanii wa nchi zote tano ambazo ni kati ya nchi sita za Afrika Mashariki.
MEA Awards, zinaanza kwa kuwa na vipengele 25, ambapo kati ya vipengele hivyo, vipengele 15 vitashindaniwa na wasanii wa nchi zote tano, huku vipengele 10 vikiwa maalum kushindaniwa na wasanii wa nchi wenyeji (host country).
Mwaka huu inaanza na Kenya, ambapo jana uzinduzi wake ulifana ukiwakutanisha wadau wa kiwanda cha burudani Afrika Mashariki. Zaidi ya MaDJ 26 walikutana kusugua santuli (CD) za mchanganyiko wa nyimbo za Afrika Mashariki. Watangazaji maarufu wa nchi hizo pia walipata nafasi ya kuchombeza yao.
Mchakato wa kuwapata washiriki wa ‘Mseto East Africa Awards’ utaanza hivi karibuni.
Kaa karibu na Dar24, tutakujuza. Bofya hashtag hizi kwenye mitandao yako ya kijamii kupata taarifa pia #MEA2018 #ConnectingEastAfrica