Hatimaye subira ya mashabiki wa Lil Wayne inafikia ukingoni wiki hii, baada ya rapa huyo kueleza kuwa albam yake mpya ya Tha Carter V itatoka rasmi usiku wa manane, Ijumaa ya Septemba 28.

Weezy amefunguka kupitia kipande cha video alichoweka mtandaoni, akisema kuwa ameamua kuchagua tarehe na muda huo ikiwa ni wakati ambapo atakuwa anasherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa (birthday).

“Kwenye birthday yangu, nina kitu maalum kwa ajili yenu. Nitakuwa naachia Tha Carter V siku hiyo. Wote mtakaokuwa na mimi, sitakuwa na cha kuwapa zaidi ya kuwashukuru wote kwa mapenzi yenu ya kila siku,” alisema Wayne anayefikisha miaka 36 wiki hii.

Aliendelea kueleza, “siku zote huwa ninajitoa kwenye mzima, lakini hii albam ni zaidi ya mimi. Mnatakiwa kukumbuka kuwa huu ni mwaka wa kazi. Huu ni mwaka wa nne, tano na sita wa kazi ambayo wote mlikuwa mnataka kuisikiliza. Ninaamini mtaifurahia. Hampaswi kuipenda, mnapaswa kuifurahia.”

Albam hiyo iliyosubiriwa kwa miaka saba tangu Tha Carter IV ilipoachiwa mwaka 2011, ilisababisha Lil Wayne kumburuza mahakamani Bosi wake Birdman mwaka 2015 akidai $51 milioni za kuvunja mkataba, sababu ikiwa kucheleweshwa kwa albam hii.

Hata hivyo, mwezi Juni mwaka huu wawili hao walipatana na kufungua njia ya kuachiwa rasmi kwa Tha Carter V ikiwa ni albam ya kwanza kutoka kwa Lil Wayne ambayo haitakuwa na nembo ya Cash Money, ikiwa ni albam rasmi ya 12 kutoka kwa rapa huyo.

Lil Wayne akiwa na mama yake

Albam hiyo imetayarishwa na Lil Wayne mwenyewe, Mannie Fresh, Mike WiLL Made-It, DVLP, DJ Mustard, Vinylz na Boi-1da.

Video: Polepole ataja wabunge wengine 3 wa Chadema kuhamia CCM
Video: Mwelekeo mpya Chadema, Magufuli kuzindua Flyover