Mahakama nchini Indonesia, imemfunga Jela miaka miwili Lina Lutfiawati (33), baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka sheria na kukufuru kupitia video aliyoipakia katika mtandao wa TikTok mwezi Machi ambayo ilimuonesha akisoma sala ya Waislamu kabla ya kula Nyama ya Nguruwe.
Mahakama hiyo ya mji wa Palembang, iliyopo kusini ya kisiwa cha Sumatra, pia ilimpata kijana huyo na hatia ya kueneza habari zilizokusudiwa kuchochea chuki au uadui wa mtu binafsi au kikundi kwa misingi ya dini na kumuamuru kulipa faini ya rupiah milioni 250 ($16,249.59).
Nyama ya nguruwe inachukuliwa kuwa ‘haram’, au hairuhusiwi, chini ya sheria za Kiislamu nchini Indonesia na Lutfiawati aliomba radhi kwa umma kwa video hiyo na kueleza kushangazwa na hukumu hiyo, na kusema “Ninajua kuwa nina makosa, lakini sikutarajia adhabu hii.”
Agosti 2023, Mkuu wa Shule ya Bweni ya Kiislamu ambayo iliruhusu Wanaume na Wanawake kusali pamoja alishtakiwa kwa kukufuru na matamshi ya chuki na Indonesia ni Taifa kubwa zaidi duniani lenye Waislamu wengi.