Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi sasa ni rasmi ataondoka Paris Saint-Germain baada ya miaka miwili ya kukaa klabuni hapo, Kocha Mkuu, Christophe Galtier, ameeleza.
ESPN iliripoti mwezi uliopita Messi ataondoka PSG wakati mkataba wake utakapokamilika kipindi cha majira ya joto, huku akiwa anawaniwa na klabu ya Saudi Arabia ya Al Hilal, ambayo ni wapinzani wa timu anayoichezea Cristiano Ronaldo, Al Nassr.
Galter amewaambia waandishi wa habari kabla ya mchezo wa mwisho wa PSG wa Ligi Kuu Ufaransa dhidi ya Clermont Foot leo kuwa: “Najisikia fahari kumunoa mchezaji bora kwenye historia ya soka.
“Hii itakuwa mechi yake ya mwisho kwenye dimba la Parc des Princes, na natumaini ataagwa kwa shangwe kubwa.
“Mwaka huu amekuwa mchezaji muhimu sana kwa timu yetu. Hakuwahi kuzungumza lolote baya kwa timu.
“Mara zote alikuwa tayari kwa timu. Ulikuwa wakati bora zaidi kufanya naye kazi kwa kipindi chote alichokaa hapa.”
Messi alichangia mabao 21 na asisti 20 kwa PSG kwenye mashindano yote msimu huu.
Messi alijiunga na mabingwa hao wa Ufaransa mwaka 2021 baada ya kukaa Barcelona miaka 21.
Pamoja na Kylian Mbappe and Neymar, alisaidia PSG kushinda taji la Ligue 1 katika msimu yote miwili aliyokaa kwenye mji mkuu huo wa Ufaransa.
Hata hivyo, kutulewa mfululizo kwenye hatua ya 16 kwenye Ligi ya mabingwa, kuna maanisha kwamba, klabu hiyo bado inalisaka taji lake la kwanza la Ulaya.
Alifunga mabao 32 katika mechi 74 kwenye mashindano yote kwa PSG, pamoja na asisiti 35.