Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amemuunga mkono Lionel Messi kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2026 kutokana na juhudi zake za kujiweka fiti.

Scaloni aliyeshinda Kombe la Dunia na kikosi cha Argentina anaamini kabisa Messi anayekipiga Inter Miami kwa sasa, anaweza kuwa fiti kucheza mashindano hayo makubwa licha ya umri kwenda.

Scaloni pia amekiri kikosi cha Argentina bado kinajengwa na uwepo wa Messi mwenye umri wa miaka 36, ni muhimu kwa ajili ya taifa hilo.

Akizungumza na Bobo TV, Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 amesema: “Messi alicheza kwa moyo wake katika Kombe la Dunia lililopita mwaka jana 2022, alikuwa hawezi kuzuilika.

“Ni mchezaji mkubwa sana, mwanzoni alicheza kama mshambuliaji, sasa anacheza nafasi ya kiungo anayetoka pembeni, kiwango chake cha ajabu sana, anaweza kucheza popote anapotaka, timu inajengwa na yeye akiwemo, nafikiri anaweza kucheza timu ya taifa kwa mrefu, lakini haya yote ni maamuzi yake.”

Mara tu baada ya kuwafunga wapinzani wao Brazil katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 mapema mwezi huu, Scaloni alitoa dokezo anaweza kuachana na timu ya taifa ya Argentina, ingawa hakuna uhakika kama kocha huyo atawatema mabingwa hao wa dunia.

Real Madrid tayari imeonyesha nia yao kwa Scaloni, ikimtazama kama mbadala wa Carlo Ancelotti, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu.

Hata hivyo, inasemekana Madrid inajiandaa kumwongeza mkataba mpya Ancelotti kwa muda wva miaka miwili, kutokana na mwenendo mzuri wa timu.

Nyota huyo wa zamani wa Barcelona kwa sasa anafurahia mapumziko nje ya uwanja kwani msimu wa Ligi ya Marekani (MIS) umemalizika.

Wakati huo huo, Inter Miami inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Al-Nassr ingawa klabu hiyo imekana taarifa hiyo.

Benchikha akataa mifumo ya Robertinho
Mbombo kuikosa Azam FC kwa siku 21