Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi amewasili Ft. Lauderdale akijiandaa kwa ajili ya hafla ya utambulisho itakayofanywa na klabu yake mpya ya Inter Miami CF, Jumapili (Julai 16).
Messi aliwasili akiwa na mkewe na watoto huku klabu pia ikitoa tangazo la kuthibitisha tukio la kukaribishwa, ambalo limeitwa “The Unveil,” na litaanza saa 6 mchana Jumapili kwenye Uwanja wa DRV PNK wa timu hiyo. Mashabiki wenye tiketi za msimu mzima wa Inter Miami wataingia bure.
Katika mahojiano na Televisheni ya Argentina kabla ya kutua Marekani, Messi alisema atajitolea kwa kila kitu kwa ajili ya klabu hiyo ya MLS, ambayo imeweka rekodi ya kucheza mechi 10 mfululizo bila ushindi kufuatia sare ya 2-2 Jumapili dhidi ya D.C. United.
“Mawazo yangu na kichwa changu havitabadilika na nitajaribu, popote ni napopaswa kuwa, kujitolea kwa uwezo wangu mwenyewe na klabu yangu mpya, kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu,” alisema Messi akikiambia kipindi cha TV cha Argentina cha Llave a la eternidad.
Akizungumzia familia yake kuhamia Marekani, aliongeza: “Tunafurahia uamuzi tuliofanya. Tumejiandaa na tuna hamu ya kukabiliana na changamoto mpya, mabadiliko mapya.”
Inter Miami bado haijafanya rasmi usajili huo, baada ya kufikia makubaliano na gwiji huyo wa Argentina, ambaye alikaa kwa misimu miwili na mabingwa wa Ligue 1, Paris Saint-Germain baada ya kuondoka Barcelona.
Miami inalenga mechi yake ya Julai 21 ya Kombe la Ligi dhidi ya Cruz Azul ili Messi acheze mechi yake ya kwanza kwa klabu hiyo.
Messi atakuwa tena na kocha wake wa zamani wa Argentina na Barcelona, Tata Martino, ambaye alichukua nafasi ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwezi Juni.
Messi mwenye umri wa miaka 35, ameshinda kila tuzo kuu inayopatikana kwake wakati wa uchezaji na kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa wakati wote.
Pamoja na kutunukiwa tuzo ya Ballon d’Or kama mchezaji bora wa dunia mara saba, Messi ameshinda mataji 43, mataji 35 kati ya hayo aliyabeba akiwa Barcelona ambayo ni mataji 10 ya LaLiga, nane ya Supercopa, saba ya Copa del Reys na mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Messi aliondoka katika klabu hiyo ya Katalunya msimu wa joto wa 2021 kama mfungaji bora wa klabu akiwa na mabao 672.
Huku Barcelona ikiwa kwenye matatizo ya kifedha, Messi alilazimika kuondoka na kukaa PSG misimu miwili iliyopita, ambapo alishinda mataji ya Ligue 1 miaka yote miwili.