Uongozi wa timu ya Lipuli FC ya mjini Iringa umekamilisha mpango wa mapokezi ya wachezaji ambao wanatarajiwa kurejea mjini humo tayari kwa maandalizi ya kuendelea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Meneja wa Lipuli FC Ramadhani Kadunda amesema maandalizi ya kupokea wachezaji yamekamilika, kuanzia leo wataanza kuwapokea kwa ajili ya kambi ya maandilizi.
Kadunda amesema wanatarajia kuanza kuwapokea wachezaji leo jioni na keshokutwa Ijumaa wataanza mazoezi kwenye uwanja wa CCM Samora.
Amesema uongozi umeamua kuweka kambi mjini Iringa, ili kupata utulivu, tofauti na wangeanzia moja kwa moja jijini Dar es salaam, ambapo wanaamini kuna rapsha za hapa na pale, na huenda wasingepata uwanja mzuri kama wa Samora kwa ajili ya mazoezi.
“Kuanzia leo jioni wachezaji wataingia, mazoezi yataanza Ijumaa saa 2 asubuhi kwenye uwanja wetu wa CCM Samora, Iringa.”
“Hatutaenda Dar kwa kukurupuka, inabidi tufanye mazoezi ya pamoja kwa siku 4 au 5 ili wachezaji wazoee na tuone wamefika hatua gani kwa sababu kila mtu alikuwa anafanya mazoezi kivyake.”
Kadunda pia amewatawaka wadau wa soka mkoani Iringa kuendelea kuwa bega kwa bega na timu yao katika kipindi hiki cha maandalizi, ili kuongeza morari kwa wachezaji wao, ambao wana jukumu la kupambana na kuibakisha Lipuli FC Ligi Kuu.
“Wanairinga wasituchoke, tuendelee kuungana na nguvu kubwa inatakiwa kutoka kwao kwa sababu hata kupanda Ligi Kuu nguvu kubwa ilitoka kwao wadau wa Iringa. Yeyote mwenye uwezo anakaribishwa kuja kuongeza nguvu ili tuinusuru timu yetu.”
Lipuli FC ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 29 (mechi na pointi sawa na Mtibwa Sugar na KMC).