Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza mkakati wa chama hicho kusaidia juhudi za kukomesha mauaji wilayani Kibiti.
Akizungumza jana mbele ya waandishi wa habari, Profesa Lipumba ameeleza kuwa chama hicho kinalaani vikali vitendo vya mauaji wilayani humo yanayofanywa dhidi ya viongozi na askari wa jeshi la polisi.
Profesa Lipumba aliongeza kuwa yeye pamoja na viongozi wengine wa chama hicho watafanya ziara wilayani humo kuzungumza na wananchi pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama.
“Tutafanya ziara Kibiti ambapo tutazungumza na wananchi, wenyeviti wetu pamoja na madiwani kufahamu tatizo hili na kusaidia juhudi za kulitatua,” alisema Profesa Lipumba.
Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo mkongwe alizungumzia kuhusu mvutano ulioibuka hivi karibuni kwenye chama hicho baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini pamoja na RITA kuisajili bodi mpya ya wadhamini wa chama hicho, kitendo kilichopingwa vikali na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Profesa Lipumba alisema kuwa Bodi hiyo mpya iko kihalali kwa mujibu wa Katiba na kwamba kesi iliyofunguliwa awali Mahakamani na wajumbe wa Bodi wanaomuunga mkono Maalim Seif sio halali . Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, hakuna mwenye mamlaka ya kufungua kesi mahakamani isipokuwa Bodi halali ya Wadhamini.
Lipumba pia aliendelea kusisitiza kuwa kazi za Katibu Mkuu wa Chama hicho zitaendelea kufanywa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya hadi pale Maalim Seif atakapokubali kurejea ofisini ili ampangie majumu.