Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Novemba 18, 2021 katika Mkutano wa Saba wa Wadau wa Lishe unaofanyika kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini Tanga.

Amesema lishe bora ndio msingi wa makuzi ya kimwili na kiakili kwa watoto na husaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuwa chanzo cha ubunifu katika kazi.

Aidha Waziri Mkuu amesema madhara yanayotokana na udumavu hayana tiba, ni ya kudumu kwa kipindi chote cha uhai wa mtoto aliyeathirika, hivyo ametoa wito kwa Watanzania wote wafuate maelekezo ya wataalam wa afya na kwa pamoja washirikiane kupambana na changamoto hiyo ya udumavu.

“Vilevile, lishe bora husaidia kuimarisha kinga na afya za watu na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za matibabu kwa baadhi ya magonjwa pamoja na kuzisaidia kaya kupunguza mzigo wa gharama za matibabu au vifo miongoni mwa watoto, wanawake na watu wazima ambao ni nguvukazi.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Sambamba na hayo yote Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI iendelee kusimamia Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga kiasi cha shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa kwa wakati na kutumika katika malengo kusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema suala la lishe ndio kiini cha nguvu kazi yenye tija ndani ya Taifa hasa katika kipindi hiki cha ujenzi wa uchumi wa viwanda ulio shindani.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema watasimamia utekelezaji wa Mpango wa Lishe ikiwa ni pamoja na kutenga shilingi 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe pamoja na kuimarisha uratibu wa masuala ya lishe katika ngazi ya Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Magaidi waliotoroka Kenya wakamatwa
Beaumellle: Africa inaonewa