Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameelezea mikakati yake ya kuboresha jiji hilo, alipokuwa akiwaomba kura wananchi wa eneo hilo.  

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wiki hii, Lissu amesema kuwa endapo atachaguliwa, ataifanya Arusha kuwa jiji la viwanda na biashara ikiwa ni pamoja na kurejesha viwanda vilivyokuwepo awali.

Kwa mujibu wa Lissu, alipokuwa na umri wa miaka 15 hadi 30 aliishi katika jiji hilo na alishuhudia viwanda vingi vya matairi, nguo na bidhaa nyingine ambavyo hivi sasa havipo. Amesema wakati huo, jiji hilo lilikuwa linafahamika pia kama ‘Geneva ya Afrika’.

“Viongozi wa Afrika walipotaka kukutana walikuja kwenye jiji hilo na viongozi wa dunia walipotaka kujadili masuala ya Afrika walikuja, lakini mambo yamebadilika, hakuna mikutano hiyo,” amesema Lissu.

Lissu ameahidi kuboresha miundombinu ya utalii ili Arusha iendelee kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa Afrika, na kwamba Serikali yake itatengeneza mahusiano mazuri na nchi za kigeni ili watalii wafike kwa wingi.

Katika hatua nyingine, Lissu aliahidi kufanya mabadiliko ya kimfumo kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubadili sheria zinazonyima dhamana kwa baadhi ya makosa ya jinai ikiwemo uhujumu uchumi na ugaidi na kurejesha mchakato wa katiba mpya.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 4, 2020
Balozi Kijazi: Wahandisi mjipange