Na Allawi Kaboyo Missenyi – Kagera

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amewaomba wananchi mkoani Kagera kumpigia kura akiahidi kutatua changamoto za wakulima wa kahawa.

Lissu ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana, Septemba 22, 2020 katika Uwanja wa Mashujaa mjini Bunazi wilayani Missenyi. Pamoja na mambo mengine amesema endapo wananchi watamchagua atahakikisha changamoto zote za kahawa zinabaki kuwa historia.

“Sasa hivi kahawa haina thamani tena kwa mwanakagera, unalima mwenyewe unavuna mwenyewe lakini unapangiwa pakuuza na bei yenyewe sio rafiki, huu mkoa unapakana na Uganda ambao wao kahawa yetu wanainunua kwa bei ya juu lakini mkulima akiipeleka anaonekana kama kapeleka magendo, niwaombe mnichague haya yote yatakwisha,” amesema.

Ameongeza kuwa Vitambulisho vya Taifa, vimekuwa kikwazo kinachosababisha wakulima kushindwa kulipwa fedha zao baada ya kuuza kahawa kutokana na kutosajili namba zao za simu huku. Hivyo, akichaguliwa atatatua kero hiyo.

Tundu Lissu akihutubia wananchi mkoani Kagera, Septemba 22, 2020

Naye mgombea ubunge jimbo la Nkenge kupitia chama hicho, Bi. Kyai amesema Wilaya ya Miseenyi inakabiliwa na kero nyingi ikiwemo migogoro ya ardhi, maji safi na salama, ukosefu wa barabara, upungufu wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari; ambapo ametumia jukwaa hilo kuwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili awawakilishe bungeni kutafuta ufumbuzi wa kero hizo.

Septemba 22, mwaka huu Lissu alifanya mikutano ya kampeini katika Wilaya za Karagwe, Missenyi na Bukoba ambapo anatarajia kuendelea na kampein zake katika maeneo mengine.

Lissu: Tutabadilisha mfumo wa kiutawala
Kagera: Idadi ya watoto waliofariki kwenye ajali ya moto yaongezeka