Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antipas Lissu amethibitisha mpango wake wa kurejea Tanzania na kazi atakayokuwa anafanya nchini.

Akizungumza katika Kongamano la Kudai Katiba Mpya, lilifanyika jana Tabata mkoani Dar es Salaam, alipohudhuria kwa njia ya mtandao, Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji alisema kuwa atarejea nchini baada ya chama chake kukamilisha utaratibu wa mikutano ya hadhara.

“Tuwaandae wananchi kwenye mikutano ya hadhara, na mimi niwaahidi, tukitengeneza utaratibu wa mikutano ya hadhara, nitakuja Tanzania. Nakuja Tanzania kufanya mikutano ya hadhara sio kuja kujifungia chumbani na kufanya mikutano ya ndani. Tujiandae kwenda kwa wananchi tutapata Katiba Mpya,” alisema Tundu Lissu.

Hata hivyo, kauli ya mwanasiasa huyo inakuja wakati ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesisitiza kusitishwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari baada ya kuhitimisha siku 100 akiwa ofisini, Rais Samia aliwataka wanasiasa kuwa na subira na kwamba kwa wakati huu wanaoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara ni wabunge na madiwani kwenye maeneo yao. Pia, alivitaka vyama vya siasa kuendelea kufanya mikutano ya ndani.

Akijibu kuhusu madai ya Katiba Mpya, Rais Samia alisema kuwa anafahamu ni suala la muhimu, lakini anaomba apewe muda ili kwanza aimarishe uchumi wa nchi.

Mugalu kuivaa Young Africans
Lamine Moro: Sijui nimekosea wapi