Siku moja baada ya Mbunge wa Kilombero(Chadema), Peter Lijualikali, kuhukumiwa kwenda jela miezi sita kwa makosa ya kufanya fujo na kusababisha taharuki, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu ameibebesha lawama CCM akidai kuwa inawaandama wapinzani na kuwatengenezea kesi za kisiasa.
Amesema kuwa Lijualikali alihukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela juzi na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero na kupelekwa katika Gereza la Idete, aidha amesema kuwa wanaodhani kumfunga Lijualikali kutawafanya wananchi waipende CCM wamekosea.
“Mara tu baada ya Lijualikali kuwashinda CCM, vita dhidi yake ilianza, lengo la kesi hizi ni siasa, CCM ikishindwa uchaguzi inaanza kutumia polisi na mahakama kwaajili ya kudhoofisha upinzani,”amesema Lissu.
Aidha, Lissu aliongeza kuwa kifungo cha Lijualikali kina historia ndefu kwani alianza kukumbwa na vita kutoka serikalini baada ya kuchaguliwa kuwa diwani wa kata ya Ifakara mwaka 2012.
Hata hivyo Mwanasheria huyo wa Chadema amebainisha kuwa pamoja na kifungo hicho cha miezi sita jela, Lijualikali bado ana sifa za kuendelea kuwa mbunge kwani hajahukumiwa zaidi ya miezi sita.