Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amejibu kauli iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai aliyemtaka kurejea nchini huku akimkumbusha kuwa hana ruhusa ya Ofisi ya Bunge ya kuwa ‘huko aliko’.
Spika Ndugai alitoa kauli hiyo hivi karibuni baada ya Lissu anayetibiwa nchini Ubelgiji kuonekana akifanya mahojiano na BBC akiwa nchini Uingereza.
Mahojiano hayo yalifanyika baada ya Lissu kutoa waraka ulioenea kupitia mitandao ya kijamii, ambapo pamoja na mambo mengine alidai kuwa kuna njama ya kumvua ubunge.
Hata hivyo, Spika Ndugai alikanusha taarifa hizo za Lissu akiziita uzushi, huku akimtaka arejee nyumbani, aache kufanya kile alichokiita kuzurura.
“Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,” alisema Spika Ndugai.
Akijibu kauli hiyo, Lissu amedai kuwa Spika Ndugai hawezi kujua kama yeye amepona kwakuwa hajawahi kumtembelea alipokuwa amelazwa hospitalini, tangu aliposhambuliwa.
“Ukimuuliza leo Lissu yuko wapi sidhani kama atakuwa na jibu. Hawezi kuwa na jibu kwa sababu yeye na watu wake hawataki kumjulia hali Lissu,” Mwananchi inamkariri.
Kuhusu kutokuwa na ruhusa, mwanasiasa huyo alidai kuwa asingeweza kuomba ruhusa wakati alitoka Dodoma akiwa hajitambui na alisafirishwa kupelekwa jijini Nairobi kwa ndege baada ya kikao cha dharura ambacho Spika Ndugai pia alihudhuria.
“Katika kikao kile, iliamuliwa mimi nipelekwe Hospiali ya Nairobi na nikasindikizwa na daktari wa Dodoma na ndege ikaruhusiwa kuruka saa 6:00 usiku. Sasa hicho kibali ninachoambiwa na Spika Ndugai ni kipi,” amehoji.
“Yeye [Spika Ndugai] alikuwepo, aliniona, hicho kibali anachokisema ni kipi? Mtu aliyejeruhiwa vile anaweza kuomba kibali? Au kuniona Uingereza ndio nimepona?” Alihoji Lissu katika mahojiano maalum aliyofanya na Mwananchi.
Amedai kuwa ameweza kusafiri kutoka Ubelgiji hadi Uingereza kwakuwa ni mwendo wa saa mbili na kwamba ameruhusiwa na daktari wake kwa siku chache.
Lissu amekuwa nchini Ubelgiji tangu Januari 2018 akipatiwa matibabu kufuatia tukio la kupigwa risasi akiwa eneo la Area D jijini Dodoma, Septemba 7, 2017 muda mfupi baada ya kutoka Bungeni.