Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amejiandaa kuwasilisha mahakamani vielelezo 27 kama ushahidi wake, katika kesi ya kupinga uamuzi wa kuvuliwa ubunge wa jimbo hilo.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), atawakilishwa mahakamani na mawakili wanne ambao ni Peter Kibatala, John Mallya, Jermia Mtobesya na Fredi Kalonga.

Wanasheria hao walifungua kesi katika Mahakama Kuu, Agosti 2 mwaka huu ambayo imepangwa kuanza kusikilizwa Agosti 21.

Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji alipoenda kupatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 jijini Dodoma alivuliwa ubunge wa Singida Mashariki, Juni 28, 2019.

Spika wa Bunge, Job Ndugai aliliambia Bunge kuwa amemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage kuwa jimbo hilo liko wazi na anaweza kuitisha uchaguzi.

Spika Ndugai alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na Ibara ya 71(1)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa mbunge atapoteza sifa za kuwa mbunge endapo hatahudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika.

Kwa mujibu wa Spika, Lissu hakuwahi kuomba ruhusa au kutoa taarifa rasmi kuhusu afya yake na alipo hivi sasa, licha ya kuonekana akizunguka kwenye nchi mbalimbali na kuzungumza na vyombo vya habari.

Mabula azungumzia hasara ya mabilioni, 138 wa wizara walioburuzwa Takukuru
Fid Q awakingia kifua wasanii wa Hip Hop Tanzania