Kufuatia uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) wa nafasi ya urais unaotarajiwa kufanyika April 14, 2018, wakili wa kujitegemea, Fatma Karume amesema kuwa Lissu amempa baraka zake zote kuwania nafasi yake ya urais wa chama hicho.
Tundu Lissu, ambaye ni mwanasheria na mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hatagombea tena nafasi hiyo baada ya kumaliza mwaka mmoja wa uongozi wake.
Lissu ametumikia uongozi chama hicho kwa muda wa miezi sita tu kutokana shambulio la risasi lililotokea Septemba 7, 2017 na watu wasiojulikana na kusababisha awe katika matibabu nje ya nchi kwa muda mrefu.
Fatma ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema hakuwa tayari kugombea urais wa TLS lakini baadaye akashawishiwa na mawakili vijana akakubali.
“Yalikuwa maamuzi magumu sana kwa sababu sikutaka kugombea, nilikuwa naombwa na vijana kwamba Fatma chukuwa fomu ugombee tutakuchagua nikasema hapana nina majukumu mengi.
Fatma amesema alichukua uamuzi ya kukubali kugombea nafasi hiyo mara baada ya kujitambua kuwa kutofanya hivyo ni ubinafsi, kwa nafasi na uwezo aliyojaliwa na Mungu ni nyema akawatumikia watu kupata haki zao.
Aidha nafasi hiyo mbali na Fatma Karume inagombewa na, Makamu Rais wa TLS, Godwin Ngwilimi, Godwin Mwapongo na Godfrey Wasonga, huku Rugemeleza Nshalla akiwa amepitishwa kuwania umakamu wa urais wa chama hicho cha mawakili Tanganyika.
Lissu ameshindwa kugombea nafasi hiyo kutokana na sheria mpya zilizoongezwa kwa wagombea na kiti hiko cha Urais wa TLS, sheria mojawapo inasema mgombea wa chama hicho hatakiwi kuwa kuwa na wadhfa wowote serikalini, Lissu ni Mbunge wa Singida Mshariki hivyo sheria hiyo kwa namna yeyote inamfunga kugombea kiti hiko.