Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi nchini Kenya anadaiwa kufungua kinywa kwa mara ya kwanza jana jioni na kumpa ujumbe Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Kwa mujibu wa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Lissu amemwambia Mbowe kuwa amenusurika katika ajali hiyo ili aweze kusimulia mkasa uliomkuta, akimtaka aendeleze mapambano.
“Mwenyekiti I survived to tell the tale. Please keep up the fight” ni maneno machache aliyosema Lissu jioni hii baada ya kufumbua kinywa!
— Godbless E.J. Lema (@godbless_lema) September 9, 2017
Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake, nyumbani kwake mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka bungeni.
Kwa mujibu wa vyombo vya usalama na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kati ya risasi zaidi ya 30 zilizoelekezwa kwa mwanasiasa huyo ambaye pia ni rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), risasi tano zilimpata mkononi, mguuni na tumboni.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema kuwa hali ya Lissu inaendelea kuimarika na kuwataka wananchi kuendelea kumuombea.
“Lissu anaendelea vizuri, lakini tunahitaji maombi zaidi kwa Mwenyezi Mungu, kila mtu amuombee,” amesema Msigwa.
Jeshi la Polisi limetangaza msako mkali wa watu waliohusika kumshambulia mbunge huyo na kueleza kuwa limeongeza timu ya wapelelezi mjini Dodoma kusaidia kufanikisha kuwakamata watu waliohusika.