Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia kwa dhamana mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa Jamhuri kutaka Lissu asipewe dhamana.
Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alimtaka Lissu kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na kila mmoja wao kusaini bondi ya shilingi milioni 10.
Pia, Lissu amepewa sharti la kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kuwa na kibali maalum cha mahakama.
Aidha, Mahakama hiyo imeitaja tarehe 24 Agosti kuwa siku ambayo Lissu atasomewa mashtaka ya awali ya tuhuma zinazomkabili baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Lissu ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) anayetetewa na mawakili 18 wakiongozwa na Fatma Karume alikamatwa Alhamisi ya wiki iliyopita kwa tuhuma za kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Gambo amnyooshea kidole Lema, amtahadharisha
- Muasisi wa jina ‘Bongo Flava’ aanzisha kipindi cha historia ya Muziki huo
Upande wa Jamhuri ulieleza kuwa Lissu alifanya kosa hilo Julai 17 katika mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.