Baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa chama cha wanasheria cha Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ameanza kutaja mikakati yake na kusema kuwa jukumu lake la kwanza litakuwa ni kutetea, kulinda haki na maslahi ya mawakili nchini.
Lissu ambaye alishinda uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 84, katika uchaguzi uliofanyika jijini Arusha jumamosi iliyopita, ameyasema hayo wakati akizungumza na Gazeti la Nipashe.
Amesema kuwa jambo la kwanza ni kuhakikisha mawakili wanaheshimiwa kila wanapokuwa kazini na kuhakikisha nchi inalinda na kufuata Utawala Bora na Sheria, kuheshimu haki za binadamu na masuala yote yaliyopo kwenye sheria iliyoanzisha TLS.
“Kumekuwa na matendo ya muda mrefu ya ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu, pia katiba katika maeneo mengi inavunjwa kwa kipindi hiki,nitasimama kikamilifu kuweza kuitetea,”amesema Lissu.
Aidha, amesema kuwa watawasisitiza wanachama wao wasinyamaze pindi watakapoona haki zao za msingi zinapokonywa.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Singida amesema kuwa chini ya utawala wake ndani ya chama hicho hautanyamazia ukiukwaji wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu.