Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema kuwa atarudi nchini, Septemba 7, 2019 ili aweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyia mwishoni mwa mwaka huu.
Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 nyumbani kwake eneo la Area D, jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka Bungeni amesema kuwa baada ya kukamilisha matibabu yake Juni mwaka huu atahakikisha anarudi nchini kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake za kisiasa.
“Nitatua tarehe saba mwezi septemba 2019 kwenye ardhi ya Tanzania kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa… nitakuwepo,” amesema Lissu alipozungumza na ‘Chadema TV’ inayorushwa mtandaoni.
Ameeleza kuwa mapokezi yake yataratibiwa na vyombo vya ndani vya chama hicho.
Aidha, Aprili 18, 2019 Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa, Mei 14, 2019 alipimwa urefu wa miguu ili atengenezewe kiatu maalum kwa ajili ya mguu wa kulia kwa sababu ya majeraha makubwa aliyoyapata.
Kadhalika, Mbunge huyo ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Wapinzani Bungeni amesema kuwa ataendelea kusikiliza ushauri wa madaktari wake kuhusu uhakika wa afya yake na safari yake ya kurejea nyumbani Tanzania.
Lissu anapatiwa matibabu nchini Ubelgiji, nchi aliyoenda kutibiwa baada ya kupata matibabu ya awali jijini Dodoma na baadaye jijini Nairobi nchini Kenya.