Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) jana alifanikiwa kupewa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuridhia hoja zake za kuomba dhamana dhidi ya pingamizi lililowekwa na mawakili wa Serikali.

Lissu ambaye alikamatwa, kusafirishwa kutoka Singida hadi jijini Dar es Salaam  ambapo alihojiwa na kulala rumande, na kisha kupandishwa kizimbani chini ya ulinzi mkali akituhumiwa kwa makossa ya uchochezi, alifanikiwa kuwazidi kete mawakili wa Serikali baada ya kupangua hoja zao ikiwa ni pamoja na sheria waliyoitumia kuiomba Mahakama kumnyima dhamana.

Lissu aliieleza Mahakama hiyo kuwa Sheria iliyotumiwa na Mawakili hao ilikuwa ya Afrika Kusini na kwamba ni sheria ya Mwaka 1976, ambayo ilitumika wakati ambao nchini humo kulikuwa na Sera ya Ubaguzi wa rangi.

Upande wa utetezi ulifanikiwa kumshawishi Hakimu ambaye alimtaka Lissu kujidhamini mwenyewe kwa kiasi cha shilingi milioni 10.

Awali, mawakili wa Serikali jana walijikuta wakimuomba mwanasheria wa Tundu Lissu, Peter Kibatalla kuwa shahidi upande wao dhidi ya mteja wake, jambo ambalo lilizua kizazaaa.

Mawakili hao wa Serikali walitoa hoja hiyo kwa madai kuwa Kibatala ndiye aliyekuwepo wakati Lissu anatoa kauli walizodai ni za uchochezi, hivyo wakamtaka awe shahidi wao na kwamba hatakiwi kumtetea Lissu.

“Mnanilazimisha niwe shahidi wenu!? Siyajui hayo maneno na sikuwepo wakati huo mnaodai Lissu aliyasema,” Kibatala anakaririwa.

Hakimu alitupilia mbali ombi hilo la upande wa Serikali na kesi imeahirishwa hadi Agost 19 mwaka huu baada ya Tundu Lissu kukana mashtaka matatu ya uchochezi yaliyosomwa dhidi yake.

Mwakyembe atetea Serikali kukata rufaa ndoa za utotoni
Video: Mkazi wa Mabibo akilalamikia kiwanda cha NIDA mbele ya Waziri