Mgombea urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania, serikali yake itaweza kuigawa Tanzania  kwa mfumo wa majimbo hasa upande wa utawala ili kila jimbo liwe na kiongozi wake anayechaguliwa na wananchi husika.

Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni alioufanya jana Septemba 22 katika uwanja wa mashujaa mjini Bunazi wilayani Missenyi Lissu amesema kuwa wananchi wa maeneo ya mipakani wamekuwa wakisumbuliwa kwa kigezo cha uraia jambo ambalo amedai linatokana na mfumo wa kiutawala uliopo.

“Mkituchagua sisi CHADEMA tutabadilisha katiba na kuleta katiba mpya, tunataka Tanzania kubadilishwa mfumo mzima wa kiutawala ili kila sehemu ama kila mkoa uwe na kiongozi wake anayetokana na wananchi wenyewe asiwe wa kuteuliwa na Rais, mfano mkuu wa wilaya achaguliwe na wananchi ili akichemka wananchi wenyewe waweze kumuondoa,” amesema Lissu.

Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Nkenge kupitia chama hicho Bi Kyai amesema wilaya ya Misenyi inakabiliwa na kero nyingi ikiwemo migogoro ya ardhi, maji safi na salama, ukosefu wa Barabara upungufu wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari ambapo ametumia jukwaa hilo kuwaomba wanankenge kumchagua ili kuweza kusaidia kutatua kero hizo.

Juzi Septemba 21, Mgombea urais kupitia Chama cha mapinduzi (CCM), Dokta John Magufuli, akihutubia mkutano wa kampeni wilayani Urambo, mkoani Tabora aliwataka wananchi kutochagua chama ambacho kina sera ya kuanzisha mfumo wa majimbo kwani utawala wa majimbo unaweza kuleta mafarakano , utengano wa kimaeneo na kufanya nchi ivurugike .

Lissu yupo mkoani Kagera akiendelea na mikutano ya hadhara ya kampeni kuomba ridhaa kwa wananchi kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania.

Miundombinu yarahisisha huduma ya damu salama
Lissu aahidi neema kwa wakulima Kagera