Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Tixon Nzunda ameitaka Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuwa chanzo cha elimu bora ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Nzunda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua rasmi kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA na kubainisha kuwa ni wakati sasa wakala hiyo kuwa chanzo cha kuwashauri wafugaji na kutoa maarifa kwa wadau wa sekta ya mifugo ili sekta hiyo iweze kuimarika na kuwa ya kisasa zaidi.
Aidha, katibu mkuu huyamefafanua kuwa wajibu wa LITA ni kuwa karibu na umma kwa kutoa huduma bora ikiwemo ya wanafunzi wanaohitimu kuwa bora na wanaoheshimika, kutambulika, wenye maarifa, wanajiamini na kuandaliwa vizuri kwenda kusaidia sekta binafsi.
Awali Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA Dkt. Pius Mwambene, akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao hicho amesema wakala hiyo imeendelea kuimarisha mahusiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kufundishia.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wafugaji wanapata mwongozo wa ufugaji bora, LITA imeanisha utaratibu wa kuwashikiza wanafunzi wa hatua ya nne kwa wafugaji katika maeneo yao wakati wa likizo ili kuanza kujenga uzoefu ujasiri wa kuwahudumia wafugaji mapema.
Kufuatia malengo hayo amewataka wajumbe wa baraza kushiriki kikamilifu na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya wakala.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema wataendelea kusimamia maadili na weledi kwa wafanyakazi wa LITA na kuongeza ushirikishwaji ili kuwa na matokeo makubwa yenye maslahi mapana yatakayoleta tija.
Amesema kuwa kila mfanyakazi aliyepo LITA atahakikisha anapata stahiki zake ili aweze kutekeleza majukumu yake kama anavyotegemewa katika kutoa mafunzo ya elimu bora ya mifugo kwa wanafunzi.
Nao baadhi ya wajumbe wa baraza katika kikao hicho, wametoa maependekezo kadhaa ya kuboresha utendaji kazi pamoja na mazingira ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa morali na kufikia malengo ya LITA.
Wamesema kikao hicho ni muhimu katika kukumbushana utekelezaji wa mambo mbalimbali yakiwemo ya kiutawala kwa kuwashirikisha wafanyakazi na kutatua kero na kuwapatia taarifa sahihi kwa wakati ili kuondoa manung’uniko kazini.