Mkufunzi wa Waamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ Leslie Liunda ameweka wazi kuwa hawawezi kumtetea mwamuzi yeyote aliyefanya makosa katika kutafsiri sheria 17 za mchezo wa Soka.
Liunda ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, ametoa kauli hiyo alipozungumza na Ligi Kuu TV ambapo amesema kamati yake ikibaini kuna Mwamuzi/Waamuzi amekwenda/wamekwenda kinyume na utaratibu itachukua hatua stahiki dhidi yake/yao.
Hata hivyo Mwamuzi huyo wa zamani katika soka la Bongo na Kimataifa amesema , kamati yake pia haitaa kimya pale mtu yeyote atakapoamua kupotosha ukweli kwa lengo la kumchafua mwamuzi aliyetekeleza vema majukumu yake na kwa usahihi.
Ufafanuzi huo umetolewa na Liunda, baada ya kuibuka Sintofahamu ya maamuzi ya kukubaliwa kwa bao la Kiungo kutoka nchini Zambia na Klabu ya Simba SC Clatous Chotta Chama wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya Kwanza siku ya Jumapili (Februari 06), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mwamuzi wa Omary Mdoe aliyechezesha mchezo huo amelalamikiwa kwa kukubali bao la Simba SC, kwa madai halikua halali kutokana na Mshambuliaji Medie Kagere kuwa eneo la kuotea kabla ya kupokea pasi kutoka kwa Pappe Ousman Sakho.
Waamuzi wengine akiwepo Hussein Athuman aliyechezesha mchezo wa Young Africans dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya bila kufungana, naye analalamikiwa kwa madai ya kuwanyonga WANANCHI katika matukio kadhaa ya mchezo huo uliounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Young Africans kupitia Idara yake ya Habari na Mawasilino pamoja na Wazee wa Klabu hiyo ni sehemu ya waliolalamika wazi kuhusu waamuzi hao na wengine ambao wanadaiwa kushindwa kuitendea haki timu yao.