September 13, 2022 ni siku ya kipekee kwa Wananchi wa Kenya ambapo wanashuhudia uapisho wa Rais Mteule, William Ruto ambaye anachukua nafasi ya Uhuru Kenyatta aliyeongoza Nchi hiyo kwa mwaka 10.
Uapisho huo unachukua nafasi katika Uwanja wa Kasarani na Wafuasi wa Rais Mteule William Ruto tayari wamefika katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi kushuhudia kiongozi huyo akiapishwa.
Kufikia saa kumi na moja asubuhi, picha kutoka uwanja huo zilionyesha maelfu wakiwa wamejaza karibu uwanja wote wenye nafasi ya watu 60,000 huku jukwaa nalo likiwa na uwezo wa kukaliwa na waheshimiwa 2500.
Katibu katika wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho alikuwa ametangaza kuwa uwanja huo utafunguliwa saa kumi asubuhi, Hata hivyo, wafuasi waliosisimka baada ya Ruto kushinda uchaguzi walianza kuingia humo saa nne usiku.
“Tulifika hapa saa tano, sisi ni miongoni mwa wale walifika mapema. Kwa sasa ni kama uwanja umejaa. Sisi hatukutaka kufungiwa nje, lazima macho yangu yaone moja kwa moja Hustler akiinua Biblia,” Michael Muiruri kutoka Ngarariga,”
“Hii ndio maana kamili ya “lero ni lero”. Hivi ndivyo mambo yalivyo uwanja wa Kasarani 5am!” Wahome alitania wapinzani wao.
Shughuli rasmi zinatarajiwa kuanza saa nne asubuhi ambapo wageni wote wakiwamo marais kutoka nje wanatarajiwa kuwa wameketi na Jaji Mkuu Martha Koome na msajili wa mahakama Ann Amadi pamoja na majaji wengine wa mahakama ya Upeo watafika saa tano, Watafuatwa na naibu rais mteule Rigathi Gachagua na mkewe akifuatwa na Ruto na Rachael.
Rais Uhuru Kenyatta atafika na kuzunguka uwanja wa Kasarani kuwaaga Wakenyana atakagua gwaride la heshima mara ya mwisho na kisha kuketi na maombi kuanza.
Wakati huo huo zaidi ya watu watano wamekimbizwa hospitalini baada ya umati wa watu kutumia nguvu kuingia uwanjani Kasarani kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais mteule William Ruto.
Maafisa wa usalama waliokuwa wakisimamia lango hilo walielemewa na kundi kubwa la watu waliojitokeza kushuhudia hafla hiyo moja kwa moja.
Maafisa wa huduma za dharura kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu waliwakimbiza majeruhi katika hospitali iliyoko karibu kufanyiwa huduma ya kwanza.
Zaidi ya maafisa 10,000 wapo kulinda usalama katika uwanja huo “Ili kuepusha changamoto za vifaa, hii ni kuomba umma kufanya mipango mbadala ya kutazama sherehe hii nyumbani kwao,” msemaji wa polisi, Bruno Shioso alisema katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Septemba 13 asubuhi.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushuhudia uapisho huo akiwa katika uwanja wa Kasarani na ataongozana na viongozi kadhaa ambao ni Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.