Klabu ya Liverpool ni miongoni mwa Klabu zilizoingia vitani dhidi ya Real Madrid kuiwania huduma ya mshambuliaji wa Paris St-Germain, Kylian Mbappe, dirisha hili ama lijalo.
Ili kumsajili fundi huyu dirisha hili, PSG inahitaji kupewa zaidi ya Euro 300 milioni kama ada ya uhamisho jambo ambalo limesababisha timu nyingi zinazomhitaji kurudi nyuma.
Mbappe ambaye kwa mwaka mmoja anapata zaidi ya Pauni 170 milioni kutokana na mshahara wake na bonasi ya usajili tayari ameshawaambia mabosi wa PSG hana mpango wa kuendelea kusalia kwenye timu baada ya msimu ujao kumalizika.
Mkataba wa staa huyu ilikuwa umalizike mwaka 2025, lakini kulikuwa na kipengele kinachomruhusu kuondoka mwakani ikiwa angependa kufanya hivyo, na ndio amekitumia kuhakikisha anaondoka.
Licha ya uwepo wa Liverpool, hadi sasa timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kuipata huduma yake ni Madrid ambao hapo kabla iliwasilisha ofa ya kutaka kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Pia Man United imetajwa endapo itanunuliwa na matajiri Waarabu, watahakikisha Mbappe anatua klabuni hapo kwa gharama yoyote ile ili kumchomoa PSG.