Majogoo wa jiji la Liverpool wametuma ofa kwenye klabu ya AS Roma ya Italia, kwa ajili ya kumsajili mlinda mlango kutoka nchini Brazil Alisson Ramses Becker.
Liverpool wametuma ofa ya Pauni milioni 62, ambayo wanaamini itatosha na kukubaliwa kumng’oa mlinda mlango huyo, ambaye aliidakia timu yake ya taifa ya Brazil wakati wa fainali za kombe la dunia zilizomalizika nchini Urusi mwishoni mwa wiki lililopita.
Wakati Liverpool wakithibitisha kutuma ofa mjini Roma-Italia, mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid nao wanahusishwa katika uhamisho wa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25.
Alipoulizwa mkurugenzi wa michezo wa AS Roma Monchi kuhusu kutumwa kwa ofa hiyo, amesema mpaka jana usiku walikuwa hawajaipokea, lakini akasisitiza kama ipo njiani wapo tayari kuipokea kwa mikono miwili, na baadae watatoa majibu ya kuikubali ama kuikataa.
Hata hivyo mwandishi wa habari wa Sky Sport Italia Gianluca Di Marzio dakika chache baadae alithibitisha kupokelewa kwa ofa hiyo na kusema: “Alisson anakaribia kutua Merseyside”.
Alison amekua na klabu ya AS Roma kwa miaka miwili, akitokea nchini kwao Brazil alipokua akiitumikia klabu ya Sport Club Internacional, na alianza kutajwa katika vyombo vya habari katika harakati za kuihama klabu hiyo, kufuatia uwezo wake mkubwa aliouonyesha wakati wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2017/18.
Endapo atasajiliwa na Liverpool kwa ada iliyowasilishwa kwenye ofa iliyotumwa mjini Roma, ataweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyeuzwa kwa pesa nyingi klabuni hapo.