Majogoo wa jiji Liverpool huenda wakaingilia kati dili la usajili wa beki kutoka nchini Senegal na klabu ya SSC Napoli ya Italia Kalidou Koulibaly.
Taarifa kutoka mjini Naples zinadai kuwa beki huyo anaewaniwa na klabu ya Man Utd, anahitajia kuondoka SSC Napoli mwezi Januari 2019, lakini ofa iliyowasilsihwa na klabu hiyo ya mjini Manchester ya Euro milioni 90 imekataliwa.
Man Utd wamejizatiti kumsajili beki huyo mwenye umri wa miaka 27, lakini taarifa za kuingia kwa Liverpool zitawafanya kukubali upinzani wa kumpata beki huyo, ambaye tayari ameshaitumikia SSC Napoli katika michezo 131 na kufunga mabao manane.
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp ameonyesha dhamira ya kumuhitaji Koulibaly ili kuboresha safu yake ya ulinzi kuanzia mwezi Januari 2019, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuhakikisha msimu huu anafanya vyema zaidi ya msimu uliopita.
Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani anaamini kama atafanikiwa kumsajili Koulibaly atakua na safu ya ulinzi itakayoweza kupambana na yoyote, hasa ikizingatiwa kwa sasa ana beki kutoka nchini Uholanzi Virgil van Dijk, ambaye ameshaonyesha msaada wa kutosha.
Hata hivyo haijafahamika Liverpool wametenga kiasi gani cha fedha, ambazo zitatumika kwenye usajiali wa Koulibaly, lakini inaamika itakua ni zaidi ya Euro milioni 90, ambazo tayari zimeshakataliwa na uongozi wa SSC Napoli kutoka Man Utd.
Liverpool na SSC Napoli wamepangwa kundi moja kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu, na tayari wameshaonja vita kutoka kwa Koulibaly.