Mshambuliaji kutoka nchini Serbia Lazar Markovic amesajiliwa kwa mkopo na klabu ya Hull City akitokea Liverpool.
Markovic amekubali kuondoka Anfield kwa makubaliano ya kucheza Hull City hadi mwishoni mwa msimu huu, kwa kuamini ataweza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa mkiaka 22, alikua anakabiliwa na changamoto ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Liverpool tangu mwanzoni mwa msimu huu.
Kabla ya dili la kusajiliwa kwa mkopo na klabu ya Hull City halijakamilishwa, Markovic alikua katika hatua za kutaka kuelekea nchini Ureno kujiunga na klabu ya Sporting Lisbon.
Liverpool walimsajili Markovic mwaka 2014 kwa ada ya uhamisho wa Pauni milioni 20 akitokea Benfica.
Msimu uliopita Markovic alipelekwa kwa mkopo nchini Uturuki kwenye klabu ya Fenerbahce na alifanikiwa kucheza michezo 20.
Meneja wa Hull City Marco Silva anamfahamu vilivyo Markovic baada ya kumfuatilia akiwa kwenye ligi ya nchini Ureno, ambapo alikua akikinoa kikosi cha Estoril.