Hatimaye majogoo wa jijini Liverpool, Uingereza wamekamilisha dili la kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji, Christian Benteke Liolo kwa ada ya usajili wa paund milioni 32.5 akitokea Aston Villa.

Benteke amejiunga na Liverpool kama suluhisho la kumaliza utata wa ushambuliaji huko Anfield, baada ya kuondoka kwa Raheem Sterling aliyetimkia Man City mwanzoni mwa juma hili.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, ameondoka Villa Park huku akikumbukwa na mashabiki wa klabu ya Aston Villa kwa mambo mazuri aliyoifanyia klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kwa msimu uliopita Benteke aliifungia Aston Villa mabao 13 katika michezo 26 ya ligi kuu ya soka nchini England aliyocheza na alikua sehemu ya kikosi kilichoifikisha kwenye hatua ya fainali ya kombe la FA The Villian kabla ya kufungwa na Arsenal mabao manne kwa sifuri.

Hata hivyo Benteke alikua mwiba kwa Liverpool katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la FA msimu uliopita, kwa kufunga moja ya mabao mawili yaliyoizamisha klabu hiyo ya Anfield.

Mara baada ya kukamilisha mpango wa usajili ndani ya klabu ya Liverpool, Benteke alizungumza na kituo cha televisheni cha klabu hiyo na kuelezea furaha yake.

Alisema ni faraja kubwa sana kwake kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool na anaamini ushirikiano mzuri atakaoonyeshwa na wachezaji wengine klabuni hapo utatoa fursa nyingine kwa The Reds kurejea kwenye makali yake kama ilivyokua siku za nyuma.

Kwa ujumla Benteke aliitumikia klabu ya Aston Villa katika michezo 101 na kubahatika kufunga mabao 49.

Katika kipindi hiki Benteke anakua mchezaji wa pili kusajili kwa thamani kubwa ya pesa nchini Uingereza baada ya usajili wa mshambuliaji Raheem Sterling kuchukuliwa na Man City kwa kiasi cha paund million 49.

Kwa Liverpool, anakuwa mchezaji wa pili kwa kusajiliwa kwa gharama kubwa baada ya usajili wa mshambuliaji Andy Carroll uliofanywa mwaka 2011 akitokea Newcastle Utd kwa kiasi cha paund milioni 35.

Man City Wajitia Kitanzi Kwa Kevin De Bruyne
Esteban Cambiasso Akataa Kuendelea Na Leicester City