Klabu ya Liverpool inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Manchester City, Kalvin Phillips, ili kuziba mapengo ya Fabinho na Jordan Henderson wanaotarajiwa kuondoka dirisha hili la usajili.
Phillips mwenye umri wa miaka 27, si miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Manchester City, lakini haionekani kuwa anauzwa licha ya Liverpool kuonyesha nia ya kumuhitaji kutokana na namna asivyokuwa tegemeo kikosini kwake.
Kiungo huyu wa kimataifa wa England ambaye msimu uliopita alicheza mechi 21 za michuano yote ambazo nyingi aliingia akitokea benchi, hata yeye ameonyesha nia ya kutaka kuondoka kikosini ili kwenda kupata nafasi ya kucheza sehemu mahali pengine tofauti na ilivyo sasa.
Katika dirisha lililipita la majira ya baridi kulikuwa na baadhi ya timu zilizoonyesha nia ya kutaka kumsajili kwa mkopo, lakini Manchester City ilikataa kumuachia supastaa huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Mbali ya Fabinho na Hederson, Liverpool imeondokewa na mastaa kibao katika dirisha hili ambao mikataba yao imemalizika, miongoni mwao wakiwamo ambao walikuwa wakipangwa kikosi cha kwanza na kuipa matokeo uwanjani.
Kwa sasa timu hiyo inapambana kujijenga baada ya msimu uliopita kuishia nafasi ya tano kwenye msimo wa Ligi Kuu England.