Majogoo wa jiji Liverpool wanajipanga kuwasilisha ofa ya kutaka kumsajili kiungo kutoka Armenia na klabu ya Borussia Dortmund ya nchini Ujerumani, Henrikh Mkhitaryan.

Liverpool wametenga kiasi cha paund million 15, ambacho wanahisi kinatosha katika mpango wa usajili wa kiungo huyo ambaye ameonyesha kuwa muhimili mkubwa kwenye kikosi cha Borussia Dortmund tangu aliposajiliwa mwaka 2013 akitokea nchini Ukraine alipokua akiitumikia klabu ya Shakhtar Donetsk.

Hata hivyo mipango ya Liverpool huenda ikagongana na ile ya klabu ya Juventus ambayo imeripotiwa kuwa katika harakati za kumuwania Mkhitaryan katika kipindi hiki cha usajili.

Mkhitaryan mwenye umri wa miaka 26, aliwahi kueleza dhamira yake ya kutaka kuondoka nchini Ujerumani alipozungumza na vyombo vya habari mwanzoni mwa mwaka huu.

Alisema anahitaji kubadili mazingira ya soka lake, baada ya kuwa sehemu ya mafanikio aliyoyavuna kwenye klabu ya Borussia Dortmund ambayo ameshaifungia mabao 14 katika michezo 60 aliyocheza.

Diamond Na Wema Sepetu Waanza Kumpigania Magufuli Kwa Vitendo
Madrid Yajihami Kwa De Gea Wa Man Utd