Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini(TARURA) imetenga Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, ambapo Wilaya hiyo imeanzishwa mwaka 2007 lakini hajaiwahi kutengewa fedha za maendeleo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha salamu za Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakati wa mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Wilaya ya Longido Oktoba 18, 2021.
“ Longido ilikuwa ikipata fedha kidogo kwa ajili ya matengenezo na kwa mwaka jana walipata mil 835 tu lakini Mtandao wa barabara wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido ni km 695 na kati ya hizo km 1.8 ni lami, km 185 ni changarawe na udongo ni km 508,” Amesema Waziri Ummy.
Aidha fedha hizo bilioni 2.2 zinakwenda kutekeleza kazi ya kujenga kilomita 1 ya lami, madaraja 8 na kupandisha hadhi barabara za udongo zenye kilometa 64 kuwa changarawe, lakini pia katika upande wa elimu Serikali pia imetenga takribani bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12 ya Sekondari na 50 katika vituo shikizi.
Akizungumza utekelezaji wa Mpango wa Elimu bila malipo, Waziri Ummy ameweka wazi kuwa katika kipindi miezi sita serikali imepeleka bilioni 3.7 kwa ajili ya elimu bila malipo katika Wilaya ya Longido huku akisisitiza Serikali kuendelea kuhudumia elimu bila malipo kote nchini.