Mamia ya wasafiri na magari yanayotumia barabara ya Morogoro – Dar es Salaam wamekwama kwa zaidi ya sita kuanzia usiku wa kuamkia leo mpaka mchana wa leo baada ya lori lenye shehena ya magogo kushindwa kupanda mlima na kufunga barabara eneo la Mikese.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim akiwa kwenye eneo la tukio leo Jumamosi Agosti 13,2022 amesema lori hilo lilifunga barabara usiku wa kuamkia leo.
Amesema jitihada zimeendelea ili kupata mashine itakayoweza kunyanyua magogo na kusogeza gari kando ya barabara.
“Mimi mwenyewe nipo hapa eneo la tukio tunachofanya kwa sasa ni kuruhusu magari kupita kwa awamu kwenye haka kamwanya kadogo angalau kupunguza foleni, maana foleni ni ndefu na hata hivyo magari yanatembea kidogokidogo,” amesema Muslimu akizungumza na mwananchi digital.
Amewataka abiria na watumiaji wengine wa barabara kuendelea kuwa wavumilivu wakati juhudi zikiendelea.