Klabu ya Los Angeles Galaxy ya Marekani inajipanga kumsajili aliyekua mshambuliaji wa Man Utd Zlatan Ibrahimovic ambaye kwa sasa yupo huru, kufuatia mkataba wake na mashetani hao wekundu kufikia kikomo mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kocha wa LA Galaxy Curt Onalfo, amekua mstari wa mbele kuushawishi uongozi wake kufanya jitihada za kukutana na wakala wa mshambuliaji huyo, ili kufanikisha mpango wa kumsajili Ibrahimovic.
LA Galaxy wamepanga kumpeleka Ibrahimovich StubHub Center kwa dau la Pauni milioni 6 kwa mwaka.
Onalfo amezungumza na wanahabari kuhusu mpango wa usajili wa Ibrahimovich na kusema – “Sera yetu sio kuangalia mchezaji anatokea wapi na kwa kipindi gani, sisi tunahitaji mchezaji wenye uwezo wa kutusaidia wakati wote.
“Mikakati ya LA Galaxy ni kuwa na wachezaji wenye hadhi kubwa duniani ya kucheza soka, hatujali umaarufu wa mtu, bali tunaangalia anaweza kutusaidia vipi katika mipango yetu.”
Wachezaji mashuhuru duniani kama David Beckham, Steven Gerrard na Robbie Keane wamewahi kuitumikia LA Galaxy. Kwa sasa klabu hiyo ina wachezaji wengine wanaofahamika duniani kama Giovani dos Santos na Ashley Cole.
Ndoto za Ibrahimovic za kuendelea kuitumikia klabu ya Man utd, ziliyeyuka kufuatia majeraha ya misuli ya mguu aliyoyapata miezi mitatu iliyopita akiwa katika mchezo wa Europa League.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35, tayari alikua ameshahakikishia nafasi ya kuendelea kuitumikia Man Utd kwa kusainishwa mkataba mpya na Jose Mourinho, lakini changamoto ya majereha ambayo yatamuweka nje kwa kipidni kirefu yalikua kikwazo.
Ibrahimovic ambaye atafikisha umri wa miaka 36 mwezi Oktoba mwaka huu, aliifungia Man Utd mabao 28 katika michuano yote aliyocheza msimu uliopita.
Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Romelu Lukaku tayari ameshasajiliwa na Man Utd akitokea Everton kama mbadala wa Ibrahimovich.