Jiji la Los Angeles la nchini Marekani limetangazwa rasmi kuwa mshindani katika kinyang’anyiro cha kuwa mwenyeji wa michuano ya Olympic ya mwaka 2024.

Jiji hilo limepitishwa rasmi na kamati ya Olympic nchini Marekani, baada ya jiji la Boston kutangaza kujitoa katika ushindani wa majiji ya nchi hiyo, kufuatia sheria kusisitiza nchi zinazotaka kuwa mwenyeji ni lazima ziwasilishe ombi kwa kupitia jiji moja.

Baada ya kuafikiwa kwa jiji hilo kuwa sehemu ya ushindani katika harakati za kusaka nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano ya Olympic ya mwaka 2024, kamati ya Olympic nchini Marekani italiwasilisha jina la Los Angeles, sambamba na vigezo vya kushawishi ili kupewa nafasi ya uenyeji.

Jiji la Los Angles liliwahi kuwa mwenyeji wa michuano hiyo mwaka, 1932 pamoja na 1984, na kwa mwaka 2024 inaaminiwa huenda likapatiwa nafasi kama hiyo kutokana na uzoefu uliowahi kupatikana miaka ya nyuma.

Kwa mara ya mwisho Marekani waliwahi kuwa wenyeji wa michuano ya Olympic mwaka 1996 kupitia jiji la Atalanta

Majiji mengine ambayo tayari yameshapendekezwa kuwania nafasi ya uenyeji wa michuano ya Olympic kwa mwaka 2024, ni Paris (Ufaransa), Roma (Italia), Budapest (Hungary) pamoja na Hamburg (Ujerumani).

Mkutano mkuu wa kamati ya Olympic ya dunia IOC utakaofanyika mwaka 2017, umepangwa kutoka na majibu ya jiji gani ambalo litapewa ridhaa ya kuwa mwenyeji wa michuano ya Olympic ya mwaka 2024.

Ikumbukwe kwamba michuano ya Olympic kwa mwaka 2016 imepangwa kufanyika kwenye jiji la Rio de Janeiro, nchini Brazil na mwaka 2020 michuano hiyo itatimua vumbi lake jijini Tokyo nchini Japan.

Lil Ommy Wa Times Fm Aachia Toleo Jipya La ‘The Playlist Magazine’ Bure
Lescot Atimkia Aston Villa