Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi anatazamiwa kukutana na Rais wa Rwanda, Paul Kagame jijini Luanda nchini Angola kwa ajili ya kusuluhisha mzozo wa mashariki mwa DRC.
Ofisi ya rais wa Angola imesema mazungumzo hayo yanatarajia kutafanyika siku ya Jumatano Juni 6, 2022 ili kupata muafaka juu ya mzozo unaoendelea baina ya nchi hizo mbili.
Kumekuwa na matukio ya kuzuka kwa mapigano ya waasi na kitu kinachozidisha mvutano kati ya nchi hizo mbili, huku Kinshasa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Juni 4, 2022 alitoa wito wa kutatuliwa kwa mgogoro huo wa kisiasa unaoleta maafa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akiongea katika mahojiano na shirika la Utangazaji la Serikali, Rais Kagame alisema uhasama uliopo hauwezi kutatuliwa kwa nguvu pekee bali unahitaji busara kuumaliza.
Viongozi wa Afrika Mashariki, majuma mawili yaliyopita waliidhinisha kuundwa kwa kikosi cha kijeshi ili kumaliza machafuko mashariki mwa DR Congo yanayowaumiza watu wasio na hatia.